News

Music

Makala

Sokkaa

Video

» » MVUA ZAUA WATOTO WATANO, BARABARA ZAFUNGWA MORO



Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakichimba udongo chini ya Daraja la Mto Msimbazi lililopo Tabata Matumbi jana kutafuta miili ya ndugu zao waliozolewa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya jiji. Picha na Venance Nestory
Moro/Dar/Arusha
Watoto watano wamekufa maji katika maeneo mbalimbali mkoani Morogoro na mwingine Dar es Salaam jana baada ya kutumbukia kwenye mito na mashimo yaliyofurika maji ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Vifo hivyo vinafanya idadi ya watu walipoteza maisha tangu mvua hizo kubwa zilipoanza Aprili 10, mwaka huu kufikia takriban 16 na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara, makazi ya watu na mazao.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo alisema jana kwamba mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kilosa, anahofiwa kufa maji baada ya kuzama katika Mto Ludewa alipojaribu kuvuka akitokea shuleni.
Tarimo alisema hadi kufikia jana asubuhi, mwili wa mwanafunzi huyo ambaye jina lake halijafahamika, ulikuwa bado haujapatikana.
Habari kutoka Kilombero zinasema watoto wawili wa familia moja katika Kitongoji cha Godauni, Kijiji cha Mkangawalo, Tarafa ya Mngeta, wamekufa maji baada ya kutumbukia kwenye shimo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile aliwataja watoto hao kuwa ni Festo Andrew (3) na Chrisantus Mnanagali (11) na kwamba walitumbukia shimoni baada ya kuteleza walipokuwa wakicheza.
Shilogile alisema katika tukio jingine, watoto wengine wawili wa familia moja, nao walikufa maji baada ya kuzama walipokuwa wakivuka Mto Morogoro katika eneo la Mlimani.
Hata hivyo, alisema wazazi na ndugu wa watoto hao waligoma kutoa taarifa polisi na badala yake walichukua miili ya marehemu iliyokuwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Morogoro.
Taarifa zilizotolewa na Wakuu wa Wilaya za Kilombero, Kilosa, Ulanga na Mvomero, mvua hizo zimeathiri kwa kiasi kikubwa mashamba, miundombinu ya barabara, majengo ya umma na makazi ya wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hassan Masala alisema Barabara za Mlimba- Ifakara na Chita-Mbingu, zimefungwa na huduma za usafiri zimesitishwa kutokana na uharibifu huo.
Alisema tayari ameshatoa taarifa kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ili kufanya tathmini ya uharibifu wa barabara hizo na kufanya matengenezo ya haraka ili kurudisha huduma za usafiri.
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Francis Miti alisema mvua hizo zimesababisha uharibifu mkubwa katika Tarafa ya Malinyi ambako baadhi ya barabara hazipitiki.

Mwananchi Kweli

Tunakushukuru kwa kuendelea kusoma habari zetu tunakuomba kama unapatwa na tatizo lolote hapa kwenye tovuti yetu una maoni,Habari na ushauri usisite kutuandikia kwenye info@news4timeblog.com kisha tutakujibu haraka iwezekanavyo.Hasante.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments

Leave a Reply

Select Menu