News

Music

Makala

Sokkaa

Video

» » Mkuu wa Kituo cha Polisi awagonga kwa gari raia watatu



Majeruhi wa awali Joseph Malugu akiwa hospitali ya wilaya ya Kahama baada ya kuumia vibaya mguu wake na sehemu nyingine za mwili.

via gazeti la MAJIRA -- Watu watatu wamejeruhiwa vibaya baada ya kugongwa na gari ambalo lilikuwa likiendeshwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, Bw. Elia Haway. 


Majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ambapo tukio hilo limetokea juzi, katika barabara iendayo Isaka, eneo la Nyasubi. 


Mkuu huyo wa kituo alikuwa akiendesha gari lenye namba T 798 BSK, aina ya 
Toyota Rav 4, ambapo majeruhi wametambuliwa kwa majina ya Joseph Malugu (35), mkazi wa Mbulu, Bw. Fitina Majuto (20) na Cosmas Peter (21) wote wakazi wa Kahama. 


Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema Bw. Haway alianza kumgonga mwendesha pikipiki 'bodaboda' Bw. Malugu katika eneo la Zahanati ya Igalirimi.


Baada ya tuki hilo, baadhi ya watu waliizingira gari hilo lakini Bw. Haway, aliliondoa gari lake kwa mwendo kasi na kwenda kumgonga mtu mwingine Bw. Majuto, katika eneo la Mkude, ambaye inadaiwa tumbo lake lilifumuka. 

Mkuu wa Kituo cha Polisi Kahama, Elia Haway (picha: Kijukuu blog)

Mashuhuda hao waliongeza kuwa, Bw. Haway baada ya kumgonga mtu wa pili hakusimama bali aliendelea na mwendo wa kasi, kumgonga Bw. Peter katika eneo la Paradise, hadi sasa hajapata fahamu. 


"Kutokana na matukio hayo, wananchi wenye hasira pamoja na waendesha pikipiki za bodaboda, walianza kumfukuza kwa pikipiki hadi Kituo cha Polisi ambako aliteremka na kukimbilia ndani ya kituo ndipo askari waliokuwa doria wakatawanya watu kwa nguvu," walisema mashuhuda hao. 


Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Joseph Foma alithibitisha kupokea majeruhi hao ambao wamelazwa katika wodi namba moja na hali zao si nzuri.


Msukuma toroli, Fitina Majuto akiwa Hospitalini



Mtembea kwa miguu Cosmas Peter akiwa hoi hospitalini

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Pikipiki wilayani humo (UDAPI), Bw. Idsam Mapende, alifanya kazi ya ziada kuwazuia waendesha bodaboda waliotaka kuandamana akitaka wawe na subira wakati taratibu za kisheria zikiendelea. 


Akizungumza na Majira, Bw. Mapande alisema ni aibu kwa Ofisa mkubwa wa polisi kuvunja sheria na kukimbia jambo ambalo hawawezi kulifumbia macho. 


Amelitaka Jeshi la Polisi wilayani humo kutenda haki juu ya tukio hilo na wasipofanya hivyo wataitisha maandamano ya amani kudai haki ili sheria ichukue mkondo wake. 


Majira lilipomtafuta Kamanda wa Polisi mkoani humo, Evarist Mangalla ili aweze kuzungumzia tukio hilo alisema yupo nje ya ofisi, lakini aliahidi kulifuatilia na kulitolea taarifa.



Mwananchi Kweli

Tunakushukuru kwa kuendelea kusoma habari zetu tunakuomba kama unapatwa na tatizo lolote hapa kwenye tovuti yetu una maoni,Habari na ushauri usisite kutuandikia kwenye info@news4timeblog.com kisha tutakujibu haraka iwezekanavyo.Hasante.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments

Leave a Reply

Select Menu