Tanzania inaweza kuwa na serikali tatu na kuzimudu iwapo itazingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na kuachana na ubadhirifu, wizi na ufisadi kwenye fedha za umma.
Mwanazuoni nguli, Profesa Ibrahimu Lipumba, ameliambia Bunge Maalum la Katiba na kusisitiza kuwa shida si fedha bali ‘ulaji’ uliokithiri ndani ya serikali.
Alikuwa akitoa ufafanuzi wa maoni ya wachache ya Kamati Namba 10, yanayounga mkono uwapo wa serikali ya shirikisho.
Alipingana na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya kuzindua Bunge hilo pamoja na maoni ya wajumbe wengi kuwa serikali tatu ni kuongeza gharama na taifa haliwezi kuiendesha.
GHARAMA
Akipinga madai kuwa kuendesha serikali tatu itakuwa ni gharama kubwa na kusema: “Gharama kubwa tulizo nazo zinatokana na ubadhirifu, ufisadi na wizi wa fedha za umma.”
Alinukuu taarifa ya mapatio ya fedha za umma ya mwaka 2010/2013 inayoonyesha kuwa asilimia kati ya 35 na 45 ya matumizi ya serikali hayana tija, hivyo fedha zinapotea kiholela kila mwaka.
Profesa Lipumba ambaye ni mchumi aliyebobea, aliliambia Bunge kuwa gharama za Muungano zimefanyiwa uchambuzi na unaoonyesha kuwa mapato ya vyanzo vya Muungano yanakidhi matumizi ya serikali ya Muungano.
Alisema takwimu zimedhihirisha kuwa zinapatikana kuanzia mwaka 1999-2000, matumizi ya Muungano yalikuwa Sh. milioni 465 wakati mapato yalikuwa Sh. trilioni 1.8.
“Ukitazama takwimu hizo, vyanzo vya Muungano vinakidhi mahitaji ya Muungano,” alisisitiza Profesa Lipumba.
Alikosoa zaidi madai ya wengi yanayojengwa juu ya hotuba ya Rais Kikwete ya uzinduzi wa bunge hilo akieleza kuwa, bajeti ya Tanzania haitenganishi vyanzo vya matumizi ya kwa utaratibu wa serikali ya Tanganyika na ya Muungano.
“Ukweli ni kwamba kuna bajeti ya serikali moja iliyoshughulikia mambo ya Tanganyika na Muungano kwa wakati mmoja,” aliongeza Profesa Lipumba huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe.
Alikosoa muundo wa utafutaji fedha za bajeti ya Serikali ya Muungano aliosema umekuwa tegemezi kwa wafadhili bila kuweka mikakati ya kujikwamua na utegemezi.“Theluthi moja ya matumizi ya serikali hiyo ikiwa daima ni mikopo na misaada kutoka nje kwa miaka yote,” alibainisha.
BAJETI ZISIZO ZA BUNGE
Profesa Lipumba alisema inashangaza kuona kuwa fedha zinazotumiwa na serikali si zile zilizopitishwa na bunge la bajeti.
“Kimsingi serikali haitoi fedha za matumizi kugharamia maendeleo na inategemea wafadhili na mikopo. Lakini pia bajeti zinazotengenezwa na Bunge hazitekelezi,” alisema Profesa Lipumba.
Aliwaambia wajumbe kuwa bajeti inayotekelezwa ni tofauti na iliyopitishwa Dodoma.
Alitoa mfano kuwa katika mwaka wa fedha wa 2010 /2011 matumizi ya kawaida ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) yalikuwa asilimia 243 sawa na mara 2.5 ya bejeti iliyoidhinishwa na bunge.
Alitaja pia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuwa yalikuwa asilimia 146 wakati Nishati na Madini yalikuwa asilimia 130 na Ulinzi yalifikia zaidi ya asilimia 135 ya kile kilichoidhinishwa na bunge la bajeti.
KIINI CHA TATIZO
“Nasema tena matatizo yetu si kwamba tuna serikali mbili au tatu bali tatizo kubwa ni ukosefu wa misingi mizuri ya kusimamia matumizi ya fedha za umma, ubadhirifu na kukosa nidhamu ya bajeti,“ alisema Profesa Lipumba.
Aliwaambia wajumbe kuwa badala ya kufumua mapendekezo ya Tume ya Warioba wayakubali na kujenga misingi ya uwajibikaji na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.
“Suala kuwa tukiongeza serikali ya shirikisho kutakuwa na matatizo si kweli, kwani kinachokula fedha za umma ni mafisadi na mabadhirifu. Wanaotaka kuwa na serikali mbili wana ajenda ya siri ya kutuzuia tusishughulikie wabadhirifu wa matumizi wa fedha za umma,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, kazi yao kama Bunge Maalum ni kuandika Katiba inayojenga misingi ya matumizi mazuri ya fedha za umma ili serikali zote ziwajibike ipasavyo na kuwa na fedha za kutosha za kuendesha serikali ya shirikisho.
MISAMAHA YA KODI
Aliendelea kukumbusha kuhusu fedha zinazopotea kwa misamaha ya kutisha ya kodi kuwa ndiyo inayolikosesha taifa mapato pia. Alikariri taarifa ya Mamlaka ya Mapato ya mwaka 2010/11 ikisema misamaha ilifikia Sh. trilioni 11.8 fedha ambazo zilikuwa zilipiwe ushuru zilisamehewa.
“Nawasihi bila kujali vyama vyetu tuenzi mapendekezo ya wananchi yaliyoletwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kukubalina na msingi mkuu wa kuunda shirikisho lenye serikali tatu,” alimalizia Profesa Lipumba.
CHANZO: NIPASHE
No comments