Meneja wa klabu ya Chelsea Jose Mourinho, amesema mchezo wa mkondo wa pili wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya nusu fainali, dhidi ya Atletico Madrid bado upo wazi kwa timu yoyote kutinga kwenye hatua ya fainali ya michuano hiyo na kuungana na Real Madrid.
Jose Mourinho, amesema mchezo wa leo ambao utashuhudia wakicheza nyumbani jijini London, utakuwa na mtihani wa aina yake, japo anakiamini sana kikosi cha The Blues ambacho siku zote hunyimwa nafasi ya kufanya vizuri.
Mourinho, amesema mchezo wa hii leo una tofauti kubwa na ule wa hatua ya robo faionali ambapo walikutana na mabingwa wa soka nchini Ufaransa PSG, ambapo katika mchezo wa mkondo wa kwanza walikubali kufungwa mabao matatu kwa moja, lakini waliporejea nyumbani walifanikiwa kusonga mbele.
Amesema kutokana na matokeo ya sare tasa ambayo yaliyopatikana katika mchezo wa mkondo wa kwanza huko nchini Hispania juma lililopita, yanatoa faida kwa Atletico Madrid kusonga mbele endapo watafanikiwa kupata matokeo ya sare ya mabao, hali ambayo ni hatari kwa kikosi chake.
Nae beki na nahodha wa klabu ya Chelsea John Terry, ameendelea kutoa tahadhari kwa mashabiki wa soka duniani kote ambao wamekua akiibeza chelsea kila inapofika katika hatua kubwa kama waliopo sasa, kukaa tayari kuiona klabu hiyo inayomilikiwa na Tycoon wa kirusi ikitinga kwenye hatua ya fainali msimu huu.
Terry, ambae alikuwa katika hati hati ya kutocheza mchezo wa hii leo kufuatia maumivu aliyoyapata wakati wa mchezo wa mkondo wa kwanza kule mjini Madrid juma lililopita, amesema waliwahi kudharauriwa kama ilivyo sasa misimu miwiwli iliyopita lakini wakafanikiwa kutinga katika hatua ya fainali na kutwaa ubingwa.
Tayari klabu ya Real Madrid imeshatanguliwa kwenye hatua ya fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, baada ya kuwagagadua mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich mabao manne kwa sifuri katika mchezo wa mkondo wa pili uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo.
Kwa mantiki hiyo sasa Real Madrid wamesonga mbele kwa jumla ya mabao matano kwa sifuri.
No comments