
Idadi ya watu waliofariki jijini Dar es Salaam kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika Ukanda wa Pwani Mashariki imeongezeka kutoka wanane hadi kufikia 13.
Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Meck Sadiki, alithibitisha kuongezeka kwa watu waliofariki dunia kutokana na mvua hizo zilizoanza kunyesha Ijumaa ya wiki iliyopita.Hata hivyo, alisema hana taarifa kamili ya idadi ya watu walioripotiwa kuathirika na mvua hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema miongoni mwa waliokufa ni pamoja na mtoto Lainat Ramadhan (2), baada ya kutumbukia kwenye shimo lililojaa maji jirani na nyumbani kwao, juzi saa 5:00 asubuhi katika eneo la Chanika Vikorongo, alipokuwa akimfuata mama yake nje.
Pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alimtaja mtu mwingine kuwa ni Damian Damian (40), ambaye alifariki dunia baada ya kusombwa na maji alipokua anajaribu kuvuka kivuko cha Makondeko kilichotengenezwa na magogo, juzi saa 12:00 asubuhi, katika mto Ubungo, uliopo eneo la Ubungo River Side.
Alimtaja mtu mwingine kuwa ni mwokota chupa aliyetambuliwa kwa jina moja la Ibrahim (25-30), ambaye alisema mwili wake ulikutwa unaelea katika mto Ng’ombe, uliopo Ubungo Maji, saa 7:20 mchana.
Vilevile, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engerberth Kiondo, alisema mwanaume, ambaye jina lake halijafahamika (20-25), alifariki dunia baada ya kuzama katika tope wakati anaogelea katika eneo la Kisarawe II, juzi saa 10:30 jioni.
Licha ya watu kufa kutokana na mvua hizo pia baadhi ya wakazi wa jijini Dar es Salaam hawana makazi ya kuishi kutokana na nyumba zao kujaa maji, huku madaraja kadhaa, likiwamo la mto Ruvu, lililoko mkoani Pwani kufunikwa na maji na mto Mzinga, uliopo jijini Dar es Salaam kukatika.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limetoa tahadhari kwa wakazi jijini humo kuwa watulivu, hasa wasafiri wasio na safari za lazima kutulia majumbani mwao kutokana na hali ya madaraja kukatika hadi hapo watakapoarifiwa.
KAYA 1,000 ZAKOSA MAKAZI MORO
Mvua hizo pia zimesababisha zaidi ya kaya 1,000 katika Manispaa ya Morogoro kukosa makazi, huku wengine wakilazimika kulala nje kutokana na nyumba zao kubomoka kufuatia kwa mafuriko.
Maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Kata ya Kichangani, Kihonda, Kilakala pamoja na Chamwino.
Baadhi ya nyumba za wananchi hao zimeonekana zikiwa zimejaa maji kufuatia mvua hizo zinazoendelea kunyesha mfululizo.
NIPASHE lilishuhudia baadhi wananchi wakiwa nje ya nyumba zao wakiezua mabati na wengine kuamua kuhama katika makazi hayo na kwenda sehemu nyingine baada ya nyumba hizo kukumbwa na mafuriko.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wananchi waliobomokewa na nyumba, wameitupia lawama serikali kutokana na kugawa viwanja vya makazi katika maeneo, ambayo yamekuwa na mikondo ya kupitisha maji.
Mmoja wa wananchi hao waliopatwa na mafuriko hayo, Adauti Kasiana, alisema anashangazwa na serikali kugawa viwanja katika maeneo ya Kata ya Kichangani na kuweka miundombinu mbalimbali wakati eneo hilo linaonekana wazi ni lenye mkondo wa maji.
“Ushahidi ni hii mvua. Eneo karibu lote la Kata ya Kichangani ni kama mto tu, maji kila kona. Ni wazi ni mkondo wa maji, lakini serikali ndiyo iligawa viwanja hapa kipindi cha chuma,” alisema Kasiana.
Alisema pamoja na wananchi hao kukumbwa na mafuriko hayo, lakini wameshangazwa na serikali kushindwa kuwapatia msaada wa aina yoyote ile kwa waathirika wa mafuriko licha ya wengine kupoteza vitu vyao na kulazimika kuomba hifadhi kwa majirani, huku baadhi yao wakilala nje.
Steven Mgendani, alisema serikali ya wilaya inapaswa kubeba mzigo kwa wananchi hao waliokumbwa na mafuriko kwa kuwapatia huduma muhimu kwakuwa wao ndio walitoa viwanja katika maeneo hayo ili watu wajenge makazi.
Diwani wa Kata ya Kichangani, John Waziri, alisema hali ni mbaya kwa wananchi wa kata hiyo kutokana na baadhi yao kupewa hifadhi kwa ndugu na majirani baada ya nyumba zao kuanguka.
Alisema wengine wamelazimika kuishi katika shule kwa muda kutokana na serikali kushindwa kutoa misaada kwa waathirika hao wa mafuriko.
JANGWANI WALALA MISIKITINI
Wakazi wa Jagwani, jijini Dar es Salaam wamelazimika kulala katika Msikiti wa Omari bin Khatwab na katika jengo la Klabu ya Yanga, baada ya nyumba zao kukumbwa na mafuriko.
NIPASHE, ambayo ilifika katika eneo hilo na lile la Kigogo na Mkwajuni ilishuhudia wakazi hao wakiendelea kufua nguo na kusafisha nyumba kwa ajili ya kurudi katika makazi yao.
Mmoja wa wakazi wa Jangwani Mtambaani ‘A’, Shabani Ibrahimu, alisema tangu Jumamosi iliyopita wamehifadhiwa katika msikiti huo pamoja na jengo la klabu hiyo kunusuru maisha yao.
Alisema watu wengine wamekuwa wakilazimika kulala kwenye daladala zinazoegeshwa maeneo hayo.
“Nyumba yangu imeingia maji na sijaokoa hata kitu kimoja. Nimelazimika kupeleka famila yangu Kigamboni kwa ndugu zangu ili mimi niendelee kubangaiza maisha. Nalazimika kulala kwenye daladala kutokana na kuwa sehemu tuliyopewa hifadhi inajaa watu,” alisema Ibrahimu.
Elizabeth Mwanjejele alisema tangu wapate mafuriko, hawana chakula na wapo na wototo, ambao wanashinda njaa, hivyo wanaiomba serikali iwasaidie chakula.
“Tuko hapa toka Jumamosi, lakini hakuna kiongozi yeyote aliyetokea hapa zaidi ya viongozi wa dini ya Islamiya. Ndiyo walituletea juzi chakula pamoja na maji,” alisema Mwanjejele.
Ali Gongo, ambaye ni mkazi wa Kigogo, alisema nyumba aliyokuwa anaishi ni ya kupanga na tangu mafuriko yalipotokea, baba mwenye nyumba yake hajamuona.
Alisema suala la kuhama serikali, litakuwa gumu kwa kuwa wanaona serikali inataka kuwanyang’anya viwanja kitendo, ambacho hawakikubali.
MAGUFULI AWAZUIA WAHANDISI KWENDA LIKIZO PASAKA
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amewagiza wahandisi wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kufuta likizo zao za Sikukuu ya Pasaka, badala yake wafanye kazi kwa saa 24 katika maeneo yote, ambayo yamekumbwa na matatizo ya mafuriko.
Waziri Magufuli alionya kuwa atakayekiuka agizo hilo atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.
Alitoa onyo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua bodi mpya ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa).
Magufuli alisema wahandisi hao wanatakiwa kufanya kazi kwa saa 24 bila kujali kuwapo kwa sikuku hiyo.
”Hakuna mhandisi yoyote, ambaye ataenda likizo ya pasaka. Watasherehekea huko huko wakiwa wanaendelea na kazi. Na yule, ambaye atajipatia likizo, atabakia huko huko, asirudi ofisini,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema matatizo yaliyojitokeza siyo suala la miundombinu, kwani mafuriko yametokea nchini Marekani kwa muda wa wiki tatu na yalileta madhara licha ya nchi hiyo kuendelea.
Dk. Magufuli alisema serikali itajitahidi kuhakikisha miundombinu iliyoharibika inarudi katika hali yake ya usalama.
Alisema maeneo, ambayo yameharibika, wahandisi wanaendelea kufanya kazi kwa saa 24 ili kuondoa msongamano wa magari.
”Juzi kwenye daraja la Ruvu wakati magari yakiwa kwenye foleni kutokana na maji mengi yaliyokuwapo. Kuna lori liliamua kuvuka maji hayo na kusombwa na maji. Hivyo, kwa sasa hali ipo shwari,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema kwenye daraja la Mpiji, ambalo lililikatika mita 25 kwenye tuta, limeendelea kumeguka na kufikia mita 75.
Hivyo, akasema wameendelea kubeba mawe kwa ajili ya kufanya ukarabati na kwamba, mpaka sasa ni zaidi ya tani 2,000, ambazo zimepelekwa na bado zoezi linaendelea huenda leo likafunguliwa.
Alitoa pole kwa wote waliopatwa na janga la mvua na kwamba, jambo hilo halipo kwa serikali, kwani yaliyotokea ni mipango ya Mungu.
Hata hivyo, Magufuli alisema anaendelea na ziara yake katika maeneo yaliyoathirika ili kuona ujenzi wa miundombinu ukiendelea katika jiji la Dar es Salaam.
Imeandaliwa na Mary Geofrey, Enles Mbegalo, Beatrice Shayo, Pilly Nashon, Theonest Bingora (Dar) na Ashton Balaigwa (Morogoro).
CHANZO: NIPASHE
No comments