Wachezaji wa timu ya Yanga wakitoka uwanjani
WAMEWEKWA sokoni! Hiyo ndiyo lugha nyepesi ambayo unaweza kuitamka kuhusu wachezaji sita wa Yanga waliomaliza mikataba yao kuanzia Aprili 19. Wapo huru kufanya mazungumzo na klabu nyingine zozote wanazotaka kujiunga nazo bila bugudha.
Rahisi sana, hebu tazama mambo yapo hivi; wachezaji sita wa Yanga mikataba yao imemalizika tangu Aprili 19 Jumamosi ile ambayo Ligi Kuu Bara msimu wa 2013/14 ilipofika tamati na wengine haifiki Juni mwaka huu lakini kwa hesabu za kalenda ya soka la Tanzania nia kama imeisha kwani timu hiyo kwa sasa haina ratiba ya kushiriki michuano yoyote kabla ya mwezi huo.
Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), mchezaji anapobakiza miezi sita kabla ya mkataba wake kumalizika, anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine kwa nia ya kujiunga nayo na hata kuingia nayo mkataba wa kuichezea baada ya kumaliza mkataba wake.
Hii ina maana wachezaji hao wasipofanya mazungumzo na Yanga au timu nyingine yoyote kabla ya Juni wanaweza kuwa katika hatari ya kutocheza msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ambayo bingwa wake huzawadiwa Sh75 milioni.
Wachezaji ambao mikataba yao na Yanga imefikia tamati ni kipa Ali Mustapha ‘Barthez’, mabeki Mbuyu Twite, David Luhende, kiungo Athumani Idd ‘Chuji’ na straika Didier Kavumbagu.
Tofauti na wengine, Kavumbagu ameupa uongozi wa Yanga siku tatu ambazo zinamalizika leo Alhamisi saa 6:00 usiku ili aweze kuambiwa kama atasajiliwa tena au vinginevyo ili aweze kujiunga na klabu nyingine zinazomhitaji.
Kavumbagu kupona
Karibu viongozi wote wa Yanga wamekuwa mbali na zoezi la usajili labda kwa kuwa tarehe rasmi kuanza mchakato huo haijafika, lakini mmoja wao, kwa sharti la kutotajwa jina aliliambia Mwanaspoti akisema: “Wachezaji wetu sita mikataba yao imemalizika, wapo baadhi wanaohitajika kwa ajili ya kuwaongezea mikataba, lakini wengine hawataongezwa.
“Mtu kama Kavumbagu analishawishi benchi la ufundi na hata Kamati ya Usajili kumwongezea mkataba kutokana na kiwango alichokionyesha katika mechi za ligi kuu tofauti na hao wengine.
“Pia benchi la ufundi halitaki kuwa na mchezaji anayeweka maslahi mbele katika timu, wanataka mchezaji anayecheza kwa kujitoa kwa moyo mmoja na kuipa mafanikio timu.
“Wapo wachezaji wanne ambao mikataba yao huenda ikasitishwa kabla ya msimu ujao kutokana na viwango vyao kushuka haraka, ni (Haruna) Niyonzima, Rajab Zahir, (Said) Bahanuzi na Shabani Kondo.”
Ripoti ya kocha
Inaelezwa viongozi wa Yanga wamejichimbia wakiitazama ripoti ya kocha, Hans Van Der Pluijm, ili waweze kuchukua uamuzi kuhusu wachezaji hao na hadi jana Jumatano mchana walikuwa wakichekecha vichwa kuhusu uamuzi wa nani wa kupewa mkataba mpya.
Kocha Pluijm aliliambia Mwanaspoti: “Ripoti yangu ipo kwa uongozi, sasa nikizungumzia mambo yaliyomo naweza kuwa kama nawafundisha kazi, wao wataijadili na kuchukua uamuzi unaofaa, kazi ni kuandika ripoti tu wao ndiyo watendaji.”
Viongozi wa Yanga kuanzia Katibu Mkuu, Beno Njovu na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Abdallah Bin Kleb, hawakuwa tayari kuzungumzia sakata hilo.
Chanzo mwanaspoti
No comments