Dar es Salaam. Hatima ya wachezaji wawili wa kigeni wa Yanga, Didier Kavumbagu na Mbuyu Twite ipo mikononi mwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Abdallah Bin Kleb.
Mbali ya Kavumbagu na Twite, pia Mohamed Kone (Azam), pamoja na Gilbert Kaze na Yaw Berko (Simba) ni miongoni mwa nyota wa kigeni watakaofungashiwa virago msimu huu.
Habari za uhakika kutoka kwa chanzo chetu zimesema kuwa uongozi wa Yanga bado haujawaongezea wachezaji hao mikataba kwa kuhofia kuwa na idadi ya wachezaji watano wa kigeni, idadi ambayo kanuni inaruhusu klabu kusajili wachezaji wageni.
Azimio la Bagamoyo lilitaka klabu zote kusajili wachezaji watatu tu wa kigeni, lakini klabu zikaomba utekelezaji wa azimio hilo uahirishwe.
Kutokana na agizo hilo ambalo lilizihusu zaidi timu za Yanga, Simba, Azam FC na Coastal Union, TFF iliwaomba viongozi wa timu hizo kuzingatia utaratibu huo ambao unaonekana kuwakumba wachezaji hao wawili.
Hii inatokana na ukweli kuwa Yanga kwa sasa ina wachezaji watatu ambao mikataba yao inamalizika msimu ujao na mwingine katikati ya mwaka 2016.
Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima walisaini mikataba ya miaka miwili mwaka jana huku Emmanuel Okwi akisaini mkataba wa miaka miwili na nusu mzunguko wa pili wa msimu huu.
Hali hiyo inawafanya viongozi wa Yanga kushindwa kusitisha mikataba ya wachezaji hao kwa kuhofia kulipa fedha nyingi na kushindwa kuwaongezea mikataba Twite na Kavumbagu wakisubiria uamuzi wa TFF.
Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema ni vigumu kuzungumzia suala la usajili wa wachezaji hao wawili kutokana na kutokuwa na majukumu ya moja kwa moja katika usajili.
Alifafanua kuwa ugumu mwingine umetokana na sheria ya TFF ambayo mpaka sasa hawajui kama itatumika au la.
“Ni sheria ambayo inatuumiza sana sisi na hii inatokana na ukweli kuwa wachezaji wetu wengi hawataki kucheza mpira, hawautilii maanani, na hivyo inatufanya tusajili wachezaji wa kigeni, TFF kupunguza ni moja ya mikakati yao,” alisema.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya usajili wa klabu hiyo, Seif “Magari” Ahmed alisema hawajakaa kujadili suala la wachezaji hao na kutaka kuvuta subira.
Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Celestin alisema kuwa kwa sasa wanaendelea na agizo la TFF iliyopita kwani hakuna taarifa yoyote nyingine iliyotolewa kuhusiana na suala la usajili.
Mwesigwa alisema kuwa ni utaratibu kuwa kama hakuna taarifa yoyote ya kufuta agizo la kwanza, basi agizo hilo linatakiwa kufuatwa. “Sisi tumeingia madarakani tumekuwa na agizo hilo, lazima tulifuate, kwani ndiyo msimamo tulioukuta kama ilivyokuwa kwenye mali nyingine za TFF, labda kamati ya utendaji au kikao kingine chochote kitengue, lakini kwa sasa hali ndiyo hiyo,” alisema Mwesigwa.
Katibu Mkuu wa Azam FC , Idrisa Nasoro alisema:“Tunasubiri kuona, wakitulazimisha hakuna jinsi tutatekeleza.”
Aliongeza kusema: “Lakini niseme wazi kanuni hii itakuwa na athari kwa timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa ambazo kimsingi zinahitaji wachezaji bora ili ziweze kufanya vizuri.”
Kama Azam italazimishwa kupunguza nyota wake itakuwa ni ndoto kwa mshambuliaji wa timu hiyo Mohamed Kone kunusurika, kwa vile mchezaji huyo aliyesajiliwa kipindi cha dirisha dogo la usajili hakuwa na mchango wowote pia mkataba wake umemalizika.
Naye Msemaji wa Simba, Asha Muhaji alisema: ”Kama TFF italazimisha utekelezaji wa kanuni ya wachezaji watatu hatuwezi kupinga.”
mwananchi
No comments